YANGA YAIFUATA SIMBA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI

YANGA imewafuata watani, Simba SC kutinga Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Zimamoto jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi sita na mabao nane ya kufunga ikiwa haijaruhusu nyavu zake kuguswa na kuendelea kuongoza Kundi B.
Yanga ilikwenda kupumzika ikiwa tayari inaongoza kwa mabao hayo mawili, yote yakifungwa na winga wake machachari wa kulia, Simon Happygod Msuva aliyeibuka mchezaji bora wa mechi.

Simon Msuva alikosa penalti pamoja na kufunga mabao mawili leo
Msuva alifunga bao la kwanza dakika ya 11 akimalizia mpira wa adhabu wa Nahodha na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima kumtungua kipa Mwinyi Abbas.
Bao la pili na la nne kwake katika mashindano hayo alifunga dakika ya 21 akiiwahi pasi ndefu ya Thabani Kamusoko na kumtoka beki Shaffi Rajab kabla ya kumchambua tena Mwinyi Abbas.
Kipindi cha pili, Yanga ilirudi vizuri tena na kuendelea kutawala mchezo, lakini hawakuwa na bahati ya kupata mabao zaidi.
Msuva aliyefunga mabao mawili pia katika mchezo wa kwanza Yanga ikiichapa Jamhuri 6-0, alishindwa kukamilisha hat trick katika mchezo wa leo baada ya kukosa penalti kipindi cha pili.
Penalti hiyo ilitolewa na r⁠efa Waziri Shekha baada ya Msuva mwenyewe kuangushwa na beki Hassan Hajji Ali kwenye boksi.
Msuva alipiga mkwaju wa penalti ukapanguliwa na kipa Mwinyi Hamisi na kumkuta tena winga huyo wa Yanga, ambaye alipoupiga tena ukagonga mwamba kabla ya kuondoshwa kwenye hatari.
Mchezo mwingine wa Kundi A kati ya Jamhuri na Azam utafuatia Saa 2:30 usiku, wakati kesho michuano hiyo itaendelea kwa mechi za Kundi A KVZ na Jang'ombe Boys Saa 10:00 jioni na Simba dhidi ya mabingwa watetezi, URA Saa 2:30 usiku.
Yanga itarudi dimbani Jumamosi kumenyana na wapinzani wao wakuu wa mataji nchini, Azam kuanzia Saa 2:30 usiku kukamilisha mechi za Kundi A.
Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul/Hassan Kessy dk46, Mwinyi Hajji Mngwali, Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’, Justin Zulu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/Juma Makapu dk82, Juma Mahadhi/Oscar Joshua dk87, Haruna Niyonzima/Deus Kaseke dk62 na Emanuel Martin/Emmanuel Martin dk76.
Zimamoto; Mwinyi Hamisi, Yussuf Mtuba, Hassan Ali/Nyange Othman dk83, Suleiman Juma, Shaffi Rajab/Suleiman Abbad dk32, Hajji Nahodha, Hassan Saidi, Makame Mbwana, Hakim Ali/Ally Salum dk18, Ibrahim Ahmada na Hamad Vuai/Amour Hussein dk53.

No comments:

Drop your comment about this..