NI SIMBA NA YANGA JUMANNE USIKU ZANZIBAR KOMBE LA MAPINDUZI

WATANI wa jadi, Simba na Yanga watakutana Jumanne Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
Hiyo inafuatia Simba SC kushinda 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys jioni ya leo katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan.
Matokeo hayo yanaifanya Simba imalize kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Jang’ombe Boys, Taifa jang’ombe zenye pointi sita kila moja na URA yenye pointi nne. 
Ikumbukwe Yanga imeshika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya Azam walioongoza kwa wastani wa mabao baada ya kufungana kwa pinti saba kila timu.

Katika mchezo wa leo, mabao yote ya Simba SC yamefungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo moja kila kipindi.
Mavugo aliyesajiliwa Simba SC msimu huu kutoka Vital’O ya kwao Burundi, alifunga bao la kwanza dakika ya 11  kwa shuti baada ya kuukuta mpira uliorudi baada ya kuogonga nguzo ya lango kufuatia shuti la winga Shiza Kichuya aliyepokea pasi nzuri ya mshambuliaji mzawa Juma Luizio
Mavugo akafunga bao la pili dakika ya 53 kwa shuti kali tena baada ya kupokea pasi ya Kichuya pembeni kulia na kumkokota beki wa Jang’ombe hadi kwenye 18 kabla ya kufunga.
Bao hilo likawafanya Jang’ombe Boys wapoteane na kuwapa fursa Simba SC walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kutawala zaidi mchezo.
Kilichofuatia ni kasi ya mashmbulizi mfululizo langoni mwa Jang’ombe Boys na kosa kosa za mabao ya wazi hadi filimbi ya mwisho. Baada ya mchezo huo, Mavugo akachaguliwa kuwa mchezaji bora.
Nahodha Jonas Mkude akasema wamefurahi kwa ushindi huo na kuongoza Kundi A na kwamba kuelekea mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya mahasimu, Yanga hawana wasiwasi.
“Sisi tumejiandaa vizuri, ni matumaini yetu na wao wamejiandaa vizuri, mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi, baada ya maandalizi tutakutana tutacheza, utakuwa mchezo mzuri, kipimo kizuri kwetu na kwao, dakika 90 zitaamua,”.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Peter Manyika, Janvier Besala Bokongu/Vincent Costa dk78, Mohammed Hussein ‘Thabalala’,  Anbdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Hijja Ugando dk71, Muzamil Yassin/James Kotei dk46, Pastory Athanas, Laudit Mavugo/Jamal Mnayte dk55 na Juma Luizio/Moses Kitundu dk63.
Jang’ombe Boys; Hashim Ruga, Shomary Ismail, Muharami Issa, Ibrahim Said/Abubakar Ali dk72, Ali Badru, Yakoub Omar, Abdi Kassim, Khamis Makame, Hafidh Juma, Juma Ali/Ali Suleiman dk67 na Abdulsamad Ali.

No comments:

Drop your comment about this..