AZAM YAIFANYA VIBAYA YANGA,YAITANDIKA BAO 4-0 KOMBE LA MAPINDUZI.

AZAM imemaliza kileleni mwa Kundi B Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Yanga mabao 4-0 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Matokeo hayo yanazifanya timu zote zimalize na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na sare moja, lakini Azam wanakuwa juu ya Yanga kwa wastani wa mabao.
Sasa Azam itacheza na mshindi wa pili wa Kundi B katika Nusu Fainali, wakati Yanga itacheza na mshindi wa kwanza wa kundi hilo.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco, maarufu kama Adebayor kwa jina la utani akifananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Manchester City, Tottenham Hotspur za England na Togo, Emmanuel Adebayor.

Bocco alifunga bao hilo dakika ya pili tu kwa shuti kali baada ya kuukuta mpira uliopanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ baada ya shuti kali pia la kiungo Joseph Maundi.   
Baada ya bao hilo, Yanga walijaribu kufunguka kwa kuongeza mashambulizi, lakini leo safu ya ulinzi ya Azam ilikuwa madhubuti mno.
Iliweza kuokoa mipira yote ya kutokea pembeni ya Yanga na hivyo kumnyima mwanya kabisa mshambuliaji hatari wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe.
Katika dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, Yanga haikuwa na shambulizi la kutisha langoni mwa Azam, zaidi ya krosi na kona za kawaida mno, ambazo ziliokolewa kwa urahisi.
Lakini Bocco angeweza kufunga mabao matatu kama angetumia nafasi nyingine mbili nzuri na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alikosa bao la wazi pia baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga hadi kwenye sita na kupiga pembeni.   
Kipindi cha pili nyota ya Azam iliendelea kung’ara na kufanikiwa kuvuna mabao matatu zaidi.
Mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed alifunga bao la pili dakika ya 54 kwa kichwa akimzidi maarifa beki Andrew Vincent ‘Dante’ baada ya krosi ya Sure Boy.
Mahundi akafunga bao zuri zaidi kwenye mchezo huo dakika ya 80 kwa shuti la umbali wa mita zaidi ya 20 kuipatia Azam bao la tatu baada ya pasi ya Sure Boy.
Winga Mghana, Enock Atta Agyei aliyetokea benchi kipindi cha pili, akaifungia Azam bao la nne dakika ya 85 akimchambua vizuri kipa Dida baada ya pasi ya Samuel Afful aliyeingia kipindi cha pili pia.
Kwa ujumla leo Yanga ilicheza ovyo mno na Azam ingeweza kupata ushindi wa kihistoria kama ingetumia nafasi zaidi ilizotengeneza.  
kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk91, Stephan Mpondo, Joseph Mahundi, Frank Domayo/Enock Atta Agyei dk79, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Mudathir Yahya dk86 na Yahya Mohammed/Samuel Afful dk65.
Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji/Geoffrey Mwashiuya dk73, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Justin Zulu/Said Juma ‘Makapu’ dk61, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko/Deus Kaseke dk83 na Juma Mahadhi/Emmanuel Martin dk34.

No comments:

Drop your comment about this..